Monday, August 27, 2012

Manji aongeza dola 20,000 Kagame Cup, kurejea leo mchana

KAMPUNI ya Quality Group Limited, imeongeza dola za Kimarekani 20,000 zaidi ya Sh. Milioni 30 za Tanzania kwenye zawadi za michuano ya soka ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality, Yussuf Manji, ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, alimpa ahadi hiyo rais wa Rwanda, Paul Kagame wakati klabu hiyo ilipomtembelea rais huyo Ikulu ya Rwanda, Alhamisi kijiji cha Urugwiro.
Kwa dola hizo 20,000 sasa kitita cha zawadi za washindi wa michuano hiyo kinatuna hadi kufika dola 80,000 kufuatia dola 60,000 zinazotolewa na rais Kagame. Mwaka 2002, Rais Kagame aliweka rekodi ya kuwa mdhamini wa kwanza kutoa zawadi za mashindani hayo, dola 60,000 ambazo zimekuwa zikigawanywa kwa washindi watatu wa juu.
Mbali na zawadi hizo, rais Kagame pia anatoa dola 15,000 kila mwaka kwa maandalizi ya michuano hiyo na kufanya mchango wake jumla kuwa dola 75,000. Kwa mchango wake huo mkubwa, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeyapa jina la rais huyo mashindano hayo.
Mwakani, michuano ya CECAFA Kagame itafanyika mjini Kigali kuanzia Januari, kwa mujibu wa Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye.Musonye ataenda Kigali mapema mwezi ujao kukutana na viongozi wa Wizara ya Michezo kujadili zaidi kuhusu maandalizi ya michuano hiyo.
Yanga ni mabingwa wa Kombe kwa miaka mfululizo, katika fainali mbili mfululizo zilizofanyika Dar es Salaam hivyo kufanya wawe wametwaa Kombe hilo mara tano jumla na mwakani wataongozana na wapinzani wao wa jadi, Simba SC kwenye michuano hiyo.
Wenyeji Rwanda wanatarajiwa kuwakilishwa na mabingwa mara tatu wa michuano hiyo, APR, ambao mwaka huu waliambulia nafasi ya nne baada ya kufungwa na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na Polisi.
Wakati huohuo;
Yanga wanatarajiwa kurejea leo Dar es Salaam leo mchana, baada ya kumaliza ziara yao nchini Rwanda jana kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali.
Katika mchezo huo, Stefano Mwasika aliisawazishia Yanga, baada ya Fabrice kutangulia kuifungia Polisi na Nahodha Msaidizi, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akafunga la pili.
Awali Ijumaa, Yanga waliwachapa mabingwa wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati, Rayon Sport mabao 2-0 kwenye Uwanja huo huo wa Amahoro.
Siku moja kabla ya mechi hiyo ya kwanza, walitembelea Ikulu ya Rwanda, walipoalikwa na Rais Paul Kagame kupeleka Kombe la Afrika Mashariki na Kati, ambalo tangu mwaka 2002 Rais Kagame amekuwa mfadhili mkuu na mlezi wa mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment