Tuesday, June 19, 2012

WAASIRA AMSHAMBULIA ESTHER BULAYA NA KUMUITA MFWASI WA CHADEMA

MH. Stephen Waasira

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Esther Bulaya, juzi walizozana katika kile kinachoonekana kuwa ni kuwania madaraka katika Jimbo la Bunda mkoani Mara, katika uchaguzi mkuu 2015.

Sakata hilo lilitokea nje ya ukumbi wa Bunge mara baada ya kuahirishwa kwa kikao juzi usiku, ambapo Wassira alimfuata Bulaya na kumhoji kwamba kwanini alitoa maneno ya kuipinga bajeti ya Serikali.

Wassira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda (CCM)
Alimwambia Bulaya: “Mimi ndiye Mbunge wa Bunda, wewe huwezi kujifanya ndiye uliyetumwa na wananchi kuja kusema maneno ya uwongo hapa, eti unaipinga bajeti ya Serikali, ni nani aliyekutuma?”

Waziri huyo alikwenda mbali na kumwambia mbunge huyo kijana kwamba, “wewe tunakufahamu una pande mbili (upinzani na CCM) na kila siku unashirikiana na Halima Mdee (Kawe-Chadema), tunakujua kwamba uko CCM na Chadema.”

Kutokana na kauli hizo, Bulaya alijibu mapigo akimwambia Wassira kwamba yeye akiwa mbunge wa CCM ana wajibu wa kukikosoa chama chake na hakuwa mtu wa kwanza kukataa kuunga mkono bajeti hadi hapo marekebisho yatakapokuwa yamefanywa.

“Mimi nina haki ya kuzungumza ndani ya Bunge na kusema kile ninachokiamini kama mbunge, wala hakuna mtu wa kuniwekea mipaka. Halafu kama ni uhusiano na wabunge wengine mbona wabunge wengi tu wa CCM wanashirikiana na upinzani?” alihoji Bulaya.

Wakati hayo yakiendelea Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na mbunge mwingine wa Viti Maalum (CCM), Rosemary Kirigini walikuwa wakishuhudia.

Nahodha alitumia dakika chache kumsihi Bulaya kutojibu mashambulizi ya Wassira.

No comments:

Post a Comment