Friday, June 22, 2012

MGOMO WA MADAKTARI KUANZA KESHO RASMI TANZANIA NZIMA


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

SASA ni dhahiri kwamba mgomo wa madaktari nchi nzima haukwepeki kutokana na Serikali kukwepa kufanya mazungumzo na Chama cha Madaktari nchini (MAT) na badala yake kukimbilia mahakamani ikitaka kupigwa marufuku mgomo wa madaktari uliopangwa kuanza nchini kote kesho.

Hatua hiyo ya Serikali ambayo sisi tunadhani siyo ya busara, ilithibitishwa jana bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa wabunge. Kwa mshangao mkubwa wa wabunge wengi, Waziri Mkuu alisema suala la madai ya madaktari halizungumziki tena kutokana na MAT kuendelea kushikilia msimamo wake wa awali wa madaktari kupandishiwa mishahara na posho mbalimbali kwa viwango ambavyo Serikali haina uwezo wa kuvilipa.

Msimamo huo mkali wa Serikali umekifanya chama hicho cha madaktari kujibu mapigo kwa kutangaza jana kwamba kitaendesha mgomo wa madaktari usiokuwa na ukomo na kwamba kesho utafanyika mkutano jijini Dar es Salaam kuweka mikakati ya namna ya kuendesha mgomo huo. Mgogoro huo kati ya MAT na Serikali unaashiria kiama kikubwa hasa kwa wananchi wengi kutokana na kipato chao kuwa cha chini, hivyo kutoweza kumudu gharama za matibabu zinazotozwa katika hospitali binafsi.

Hakuna aliyemtazamia Waziri Mkuu kutoa kauli hiyo ambayo kwa tafsiri yoyote ile inaashiria shari, hasa baada ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Husein Mwinyi kuonyesha dhamira ya Serikali ya kutaka kushughulikia madai ya madaktari kwa njia ya majadiliano kwa kusema mapema wiki hii kuwa, Serikali ingekutana nao kujadili na kufikia mwafaka juu ya madai yao, huku akiwasihi madaktari kutofanya mgomo. Kauli hiyo ya Waziri Mkuu ambayo haikutegemewa bila shaka ndiyo imepandisha joto la mgogoro huo, huku hofu ya kufanyika kwa mgomo huo ikitanda nchi nzima.

Hali hiyo ya sintofahamu inakuja muda mfupi tangu nchi iliposhuhudia mgomo mkubwa wa wanataaluma hao mapema mwaka huu, mgomo uliosababisha mateso makubwa ambapo wagonjwa nchi nzima walilia na kusaga meno. Kishindo cha mgomo huo kiliitikisa nchi na kulilazimisha Bunge kuingilia kati na kuzirudisha pande hizo mbili kinzani katika meza ya mazungumzo. Tumeambiwa kuwa, katika kujaribu kuepusha maafa katika mgogoro unaoendelea hivi sasa, Bunge kupitia Kamati ya Huduma za Jamii, limeitaka Serikali kuchukua hatua za kuzuia mgomo wa wanataaluma hao kabla haujaanza.

Jambo linalojitokeza katika mgogoro huo usioisha ni kwamba pande zote mbili haziaminiani. Madaktari wanasema Serikali haina nia ya dhati na kwamba inashughulikia suala hilo kisiasa, huku Serikali nayo ikihisi kwamba kuna msukumo wa kisiasa katika madai hayo ya madaktari. Ndiyo maana mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamekuwa yakisuasua na kuvunjika mara kwa mara. Na pengine ndiyo maana Serikali imekuwa haitekelezi ahadi ambazo imekuwa ikitoa kwa madaktari hao na kuamua kukaa kimya.

Tulionya mara kadhaa huko nyuma kupitia safu hii kwamba mwafaka na maridhiano hayawezi kupatikana katika mazingira kama hayo ya kutoaminiana. Tulishauri kwamba katika mazingira hayo, lazima wapatikane wapatanishi wanaokubalika na kuaminiwa na pande zote zilizo katika mgogoro huo. Tulikwenda mbele zaidi na kupendekeza majina ya watu mashuhuri na waadilifu tuliodhani wanaweza kusuluhisha mgogoro huo, huku tukishauri kwamba Serikali haiwezi kuwa msuluhishi wa mgogoro huo kwa sababu nayo ni sehemu ya tatizo.

Sasa nini kifanyike ili kuepusha mgomo ambao hapana shaka utaleta mateso na vifo kwa wananchi ambao hawana hatia? Tunashauri kwamba Serikali itulie, iondoe kesi mahakamani na kwa kushirikiana na viongozi wa madaktari ihakikishe wanapatikana wasuluhishi wanaokubalika kwa pande zote mbili. Tunawashauri madaktari nao wakubali ukweli kuwa, katika kutafuta maridhiano katika mgogoro kama huo, haiwezekani wapate kila kitu wanachokitaka. Ukweli ni kwamba baadhi ya madai yao hayatekelezeki, hivyo watatakiwa kulegeza misimamo yao na ndipo wasuluhishi wataweza kutoa maamuzi yatakayoridhiwa na pande zote mbili. 

No comments:

Post a Comment