TIMU 20 KUCHEZA LIGI DARAJA LA
KWANZA
Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeridhia mapendekezo ya Kamati ya
Mashindano ya kutaka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwa na timu 20 badala ya 18 za
sasa.
Lengo la mabadiliko hayo ni
Ligi ya Taifa (NL) kuchezwa kwa kanda, hivyo msimu huu timu mbili zaidi
(ukiondoa tatu ambazo zimeshapanda kutoka NL) zitaongezwa ili kufikisha idadi ya
timu 20 katika FDL.
Timu ambazo zimepanda kutoka
NL iliyochezwa katika vituo vitatu ni; Kanembwa JKT ya Kigoma iliyoongoza Kituo
cha Kigoma, Ndanda SC ya Mtwara iliyoibuka kinara Kituo cha Mtwara na Polisi
Mara iliyokamata usukani katika Kituo cha Musoma.
Kamati ya Utendaji pia
imepitisha mapendekezo ya kuchezwa play off ili kupata timu mbili zaidi za
kucheza FDL msimu huu. Timu zitakazocheza play off katika utaratibu
utakaotangazwa baadaye na Kamati ya Mashindano ni tatu zilizoshuka kutoka FDL na
tatu nyingine zilizoshika nafasi za pili katika NL kutoka vituo vya Kigoma,
Mtwara na Musoma.
Timu tatu zilizoshuka FDL ni
AFC ya Arusha, Samaria ya Singida na Temeke United ya Dar es Salaam wakati
zilizoshika nafasi za pili katika NL na vituo vyao kwenye mabano ni Kurugenzi ya
Iringa (Mtwara), Mwadui ya Shinyanga (Kigoma) na Tessema ya Dar es Salaam
(Musoma).
Hata hivyo, timu
zitakazoshuka kutoka Ligi Kuu bado zitaendelea kuwa tatu kama ilivyo kwa
zitakazopandwa.
AWAMU YA KWANZA USAJILI
MWISHO AGOSTI 10
Kipindi cha kwanza cha
usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu wa 2012/2013 kitamalizika Agosti 10
mwaka huu kulingana na kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ya 2012/2013.
Uhamisho wa wachezaji
unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuacha
wachezaji (sio wa Ligi Kuu. Wachezaji wa Ligi Kuu wanacheza kwa mikataba) ni
kuanzia Juni 15- 30 mwaka huu.
Kwa klabu za Ligi Kuu
kutangaza wachezaji watakaositishiwa mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka
huu na usajili wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka
huu.
Tunasisitiza kipindi cha
usajili kiheshimiwe na mikoa yote kwa sababu usajili huo huo ndiyo utakaotumika
katika michuano ya Kombe la FA. Kwa maana nyingine hakutakuwa na kipindi kingine
cha usajili wa wachezaji kwa klabu zote nchini hadi hapo litakapofunguliwa
dirisha dogo.
Mechi ya kufungua msimu ya
Ngao ya Jamii (Community Shield) kati ya mabingwa wa Ligi Kuu, timu ya Simba na
makamu bingwa Azam itachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati Ligi Kuu itaanza
Septemba Mosi mwaka huu, na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) yenyewe itaanza Septemba
15 mwaka huu.
Ratiba ya Ligi Kuu itatolewa
Julai 23 mwaka huu.
MISRI YAOMBA KUIKABILI
NGORONGORO HEROES
Chama cha Mpira wa Miguu
Misri (EFA) kimeomba mechi mbili za kirafiki kwa timu yao ya vijana na timu ya
vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (Ngorongoro Heroes).
EFA imeomba mechi hizo
zichezwe Julai 3 na Julai 5 mwaka huu kwa masharti maalumu. Ikiwa zitachezwa
Misri, mwenyeji (EFA) atagharamia Ngorongoro Heroes kwa malazi, chakula, usafiri
wa ndani na sehemu ya kufanyia mazoezi.
Ikiwa mechi hizo zitachezwa Dar es Salaam,
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaigharamia timu ya Misri kwa
malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya mazoezi. Hivyo kila timu
itajigharamia kwa usafiri wa ndege na posho kwa timu yake.
Sekretarieti ya TFF inafanya
uchambuzi wa gharama ili kujua ipi ni nafuu kabla ya kufanya uamuzi wa wapi
mechi hizo zichezwe.
Ngorongoro Heroes imeingia
raundi ya pili ya michuano ya Afrika ambayo fainali zake zitafanyika mwakani
nchini Algeria baada ya kuitoa Sudan katika raundi ya kwanza.
Itacheza mechi ya kwanza ya
raundi ya pili Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano
itakuwa Agosti 11 mwaka huu nchini Nigeria.
No comments:
Post a Comment