WASANII nguli wa miondoko ya bongofleva sanjari na Machozi Band, kesho watalipamba shindano la kumsaka mrithi wa Salha Israel katika shindano la Miss Ilala litakalofanyika kwenye ukumbi wa nje wa Nyumbani Lounge uliopo maeneo ya Namanga, Dar es Salaam.
Wasanii hao ambao watatumia bendi katika kuonesha umahiri wao, wamejumuika kwenye shindano hilo ili kukidhi kile mashabiki wa Miss Ilala wanachotarajia. Mbali ya wasanii hao, msanii wa luninga, Steve Nyerere ndiye atakayeliongoza kama MC ambapo Alhamis(kesho) watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kwenye club ya City Sports Lounge kwa ajili ya kutangaza zawadi.
Vimwana 14 wanaotarajiwa kupanda jukwaani kuwania umalkia wa Kanda ya Manispaa ya Ilala, Redds Miss Ilala 2012, kati yao 12 wiki iliyopita walishindana kwenye kategoria ya kipaji ambapo watano kati yao walitinga hatua ya fainali, ambayo itamaliziwa siku ya shindano lenyewe Ijumaa.
Katika kinyanganyiro hicho mrembo Mary Chizi alikuwa kivutio zaidi kwa jinsi alivyoonesha umahiri wake wa wepesi wa kujvingirisha mwili huku Mectilda Martin akizoa ukumbi mzima kwa kurap na huku akiwa ameandana kwa kucheza hata mavazi yanayotumiwa na wasanii wa miondoko hiyo.
Magdalena Munisi hakuwa nyuma kabisa katika kumwigiza mwanamuziki nguli wa marekani, Ciara kwa umahiri wake wa kulitumia jukwaa, lakini kubwa kuliko pia kwa mrembo Amina Sangawe alibuni nguo kwa kutumia vipande viwili vya khanga ambapo aliliunganisha jukwaani kupitia pini nakumvika mmrembo mwenzie. Stella Moris kwa upande wake alionesha ukali kwa kuimba.
Warembo hao, wamekuwa wakijifua kwa takriban wiki nne sasa chini ya wakufunzi, Slyvia Mashuda ambaye ni Miss Tanzania namba mbili mwaka 2008 na Miss Ilala wa mwaka huo, na Neema Mbuya na Dickson Daudi wa THT katika shoo.
Miss Ilala, yenye rekodi ya kutoa warembo wanne waliotwaa taji la Miss Tanzania kuanzia mwaka 1999, (Hoyce Temu), 2000 (Jacquline Ntuyabaliwe aka K-Lyne), 2002 (Angela Damas Mutalimwa) na Salha Israel anayeshikilia taji hilo kwa sasa, imepania kuendeleza rekodi yake nzuri mwaka huu.
Miss Ilala inahusisha warembo kutoka vitongoji vya Dar City Center, Tabata na Ukonga na inadhaminiwa na City Sports Lounge, Redd's Premmium Cold, Uhuru One, Dodoma Wine, Nyumbani Lounge, gazeti la Jambo Leo, 100.5 Times FM, Redio ya watu 88.4 Cloud's FM.
Mbali ya walioingia tano bora katika vipaji, warembo wengine wanaoshiriki shindano hilo ni pamoja na Mary Chizi, Matilda Martin, Magdalena Munisi, Suzan Deodatus, Whitness Michael, Stella Moris na Elizaberth Pertty. Wengine ni Wilmina Mvungi, Zawadi Mwambe, Rehema Said, Diana Simon, Amina Sangwe, Noela Michael na Phillios Lemi.
Mbali ya Redd's Premmiun Cold, wadhamini wengine katika mashindano hayo ni pamoja na Uhuru One, Dodoma Wine, City Sports Lounge, gazeti la Jambo Leo, Nyumbani Lounge, 100.5 Times FM, Redio ya watu 88.4 Cloud's FM na Amaya Salon.