Kwa mara ya kwanza
kabisa katika historia ya nchi yetu kijana Wilfred Moshi, Mbongo wa kawaida tu
(anayefanya kazi ya upagazi kuwahudumia watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro),
ameweka rekodi mpya ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupanda Everest - mlima mrefu
kushinda yote duniani.
Hivi karibuni, Moshi, alialikwa majuma matano nchini
Uingereza kutembelea shule mbalimbali za Scotland akakutana na takribani
wanafunzi 5,000 .
Wanafunzi walitaka kufahamu namna alivyopanda mlima Everest wenye mita 8,848
(futi 29, 029). Mlima huu mgumu kuukwea kuliko yote ulimwenguni umewahi
kupandwa na na watu 4,000 toka ulipoanza kufikiwa kileleni na Edmund Hillary na
Sherpa Tenzig Norgay mwaka 1953. Kati ya hao 200 walifariki.
Mwaka huu wanne wameshafariki wakiijaribu shughuli hii
inayochukua miezi miwili na kugharimu Dola 100,000 (Shilingi milion 157,500,000) Linganisha na mlima Kilimanjaro unaodai siku
tano na gharama (ikiwepo vifaa husika) Dola 2,000 (Shilingi milioni 3, 161).
Wilfred Moshi ni Mtanzania wa kwanza na Mwafrika wa tatu
kufikia kilele cha kitendawili hiki Mei 19 2012 (kilichoitwa “Chomolungma” na wenyeji kabla ya
kubatizwa jina la Everest na Waingereza enzi za ukoloni) Wilfred aliyezaliwa mwaka 1979 na kumaliza
kidato cha sita shule ya Kilimanjaro Boys, amekuwa akipanda mlima Kilimanjaro
tangu angali bado shuleni na miaka 19.
Mara baada ya kuwasili Edinburgh, Scotland alikaribishwa
bungeni akakutana na Waziri wa Sheria mheshimiwa Kenneth MacAskill na viongozi
wengine. Safari ilikirimiwa na shirika la “Twende Pamoja” lililoanzishwa na
Mike Knox miaka 30 iliyopita. “Twende Pamoja” imejenga ushirikiano kati ya
wanafunzi wa Scotland na shule 34 za Kitanzania. Ni moja ya mashirika, watu
binafsi na wafadhili mbalimbali ulimwenguni waliochangia fedha za kumwezesha
Moshi kupanda mlima Everest.
Balozi wetu Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe vile
vile alisafiri toka London kumtembelea Wilfred Moshi na kumpa heko. Umbali wa
London had Scotland ni kama Dar es Salaam hadi Kigoma!
Kwanini Moshi anahusudu
kupanda milima?
Ukweli sisi bado hatuoni umaana (au umuhimu) wa kupanda milima. Anasema lengo
lake lilikuwa kutimiza ndoto ya Mtanzania wa kwanza kupanda Everest. Pili,
upandaji milima ni moja ya njia zinazoweza kusaidia kujenga jamii kwa misaada
na fadhila za mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO). Tujiulize vipi alisaidiwa
na watu wengi namna hiyo kuchangia fedha takikana? Tatu, Moshi amethibitisha
ukiwa na moyo na jitihada unaweza kufanya lolote.
Ushujaa na ushupavu wake utasaidia kuwahamasisha
Watanzania kuwa ukitaka kufanya jambo lolote lile unaweza ili mradi uwe na moyo
na nidhamu. Mpanda milima mashuhuri,
Mike Hamill, aliyeshakwea milima yote mikubwa saba duniani anasema katika
kitabu chake kipya (“Climbing Seven Summits”) wapanda milima ni watu wenye moyo
wa kufikia malengo na kufanikiwa katika maisha yao.
Akiwa Uingereza Moshi
alipanda mlima wa Ben Nevis mrefu kuzidi nchi hii- wenye mita 1,344 (futi 4,
409). Baada ya kuimudu milima mitatu sasa , Wilfred Moshi ameazimia kupanda
milima katika mabara yote 7 duniani. Anasema amebakisha milima mitano:
Aconcagua ( Marekani ya Kusini ), Kosciuszko (Australia), Vinson Massif (
Antarctica) McKinley(Alaska) na Elbrus(Urusi).
Mungu ambariki Mtanzania huyu mwenye jazba na hamasa
anayetuletea sifa.
Imeandikwa na Freddy Macha kwa ushirikiano na
Urban Pulse
Picha
zote hisani ya Wilfred Moshi na Urban Pulse