Thursday, September 6, 2012

REDDS MISS ILALA KUZOA MIL.1.5


Redd’s Miss Ilala 2012 atakayepatikana kesho, anatarajiwa kuzoa kitita cha shilingi millioni 1.5 sanjari na kupata tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki shindano la Taifa la Redd’s Miss Tanzania, linalotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

 
Mrembo huyo atakayekuwa mrithi wa Salha Israel, mshindi wake wa pili atajinyakulia kitita cha Sh.1.2 huku mshindi wa tatu akiibuka na Sh. 700,000. Zawadi hizo za pesa taslimu pia zitakwenda kwa washindi wan ne na tano ambao kwa pamoja watapata Sh. 400,000 kila mmoja ambapo warembo wengine tisa watakaosalia kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh.200,000.

 
Redd’s Miss Ilala ambayo itapambwa na wasanii nguli wa miondoko ya bongofleva nchini sanjari na B-Band watakaoshirikiana na Machozi Band, Chegge Chigunda, Banana Zahir Ally Zorro, Ommy Dimpoz na Lady Jaydee watakuwa jukwaani kuhakikisha wanakidhi kiu ya mashabiki watakaofika kesho Agosti 7, kwenye ukumbi wa nje wa Nyumbani Lounge.

 
Wasanii hao ambao watatumia bendi katika kuonesha umahiri wao, wamejumuika kwenye shindano hilo ili kukidhi kile mashabiki wa Miss Ilala wanachotarajia. Mbali ya wasanii hao, msanii wa luninga, Steve Nyerere ndiye atakayeliongoza kama MC.

 
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye shindano hilo ambalo kwa mara ya kwanza katika historia ya urembo nchini, mashabiki wa tasnia hiyo walio nje ya Tanzania watalifuatilia live kupitia mtandao wa Uhuru One, ambao kiutalaam watahikisha wana stream live shindano hilo linalotarajiwa kuwa la aina yake.

 
Mbali ya mashabiki kupata faida hiyo ya kuoneshwa moja kwa moja kupitia mtandao, lakini faida kubwa kamati ya Miss Ilala imezingatia mchango wa wadhamini matangazo yao kuonekana nje ya mipaka ya jiji la Dar es Salaam na ughaibuni kwa ujumla.

 
Vimwana 14 wanaotarajiwa kupanda jukwaani kuwania umalkia wa Kanda ya Manispaa ya Ilala, Redds Miss Ilala 2012, kati yao 12 wiki iliyopita walishindana kwenye kategoria ya kipaji ambapo watano kati yao walitinga hatua ya fainali, ambayo itamaliziwa siku ya shindano lenyewe Ijumaa.

 
Warembo hao, wamekuwa wakijifua kwa takriban wiki nne sasa chini ya wakufunzi, Slyvia Mashuda ambaye ni Miss Tanzania namba mbili mwaka 2008 na Miss Ilala wa mwaka huo, na Neema Mbuya na Dickson Daudi wa THT katika shoo.

 
Miss Ilala, yenye rekodi ya kutoa warembo wanne waliotwaa taji la Miss Tanzania kuanzia mwaka 1999, (Hoyce Temu), 2000 (Jacquline Ntuyabaliwe aka K-Lyne), 2002 (Angela Damas Mutalimwa) na Salha Israel anayeshikilia taji hilo kwa sasa, imepania kuendeleza rekodi yake nzuri mwaka huu.

 
Miss Ilala inahusisha warembo kutoka vitongoji vya Dar City Center, Tabata na Ukonga na inadhaminiwa na City Sports Lounge, Redd's Premmium Cold, Uhuru One, Dodoma Wine, Nyumbani Lounge, gazeti la Jambo Leo, 100.5 Times FM, Redio ya watu 88.4 Cloud's FM.

Mbali ya walioingia tano bora katika vipaji, warembo wengine wanaoshiriki shindano hilo ni pamoja na Mary Chizi, Matilda Martin, Magdalena Munisi, Suzan Deodatus, Whitness Michael, Stella Moris na Elizaberth Pertty. Wengine ni Wilmina Mvungi, Zawadi Mwambe, Rehema Said, Diana Simon, Amina Sangwe, Noela Michael na Phillios Lemi.

 

Mbali ya Redd's Premmiun Cold, wadhamini wengine katika mashindano hayo ni pamoja na Uhuru One, Dodoma Wine, City Sports Lounge, gazeti la Jambo Leo, Nyumbani Lounge, 100.5 Times FM, Redio ya watu 88.4 Cloud's FM na Amaya Salon.
Mratibu wa Miss Ilala, Juma Mabakila(katikati) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo katika Club ya City Sports Lounge kuhusu shindano hilo linalofanyika kesho Ijumaa katika ukumbi wa nje wa Nyumbani Lounge. Kushoto ni Meneja wa kinywaji cha Redd's, Victoria Kimaro na Mc wa shindano hilo, msanii Steve Nyerere
 

No comments:

Post a Comment