Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho
wa Kimataifa (ITC) kwa Watanzania saba kucheza mpira wa miguu katika nchi za
Kenya na Msumbiji.
TFF imetoa hati hizo kwa wachezaji hao baada ya kuombewa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu la
Msumbiji (FMF) ili waweze kucheza katika klabu za nchi hizo.
Wachezaji waliokwenda Bandari ya Kenya na klabu walizokuwa
wakichezea nchini kwenye mabano ni David Naftali (huru), Meshack Abel (huru),
Mohamed Banka (huru) na Thomas Mourice (Mtibwa Sugar).
Klabu ya CD Madchegde ya Msumbiji imewachukua wachezaji Hassan
Hassan Mustapha kutoka Mgambo Shooting ya Tanga, na Abdallah Ally Abdallah na
Thobias David Silas kutoka klabu ya daraja la kwanza ya Transit Camp ya Dar es
Salaam.
ODHIAMBO WA AZAM APATA ITC
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea Hati ya
Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mchezaji George Odhiambo, raia wa Kenya
aliyejiunga na klabu ya Azam.
Hati hiyo imetolewa na Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU)
ambapo Odhiambo alikuwa akicheza nchini humo kabla ya kutua Azam kwa ajili ya
msimu wa 2012/2013.
Klabu nyingine zinazosajili wachezaji kutoka nje ya Tanzania
zinatakiwa kuhakikisha zinakamilisha uhamisho wao (transfer) kabla ya Julai 30
mwaka huu ambayo ndiyo siku ya mwisho kufanya hivyo.
Kanuni ya 41 ya Ligi Kuu kuhusu ITC inasema: “(1) Maombi ya ITC kwa
wachezaji wa kigeni wa kulipwa yatawasilishwa kupitia mtandao wa kompyuta kwa
kutumia program ya ‘Transfer Matching System-TMS’ baada ya klabu zinazohusika
na mchezaji huyo au wachezaji hao kukubaliana nje ya mtandao.
(2) Maombi ya ITC kwa wachezaji wa kigeni wasio wa kulipwa
yatawasilishwa kwa barua TFF baada ya klabu zinazohusika na mchezaji huyo au
wachezaji hao kukubaliana. Chama cha Soka kinachotoa ITC kwa njia hii
kitapeleka nakala FIFA. (3) ITC haihitajiki kwa mchezaji mwenye umri chini ya
miaka kumi na mbili (12).”
Tunapenda kuzikumbusha klabu kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 53 ya Ligi
Kuu, wachezaji wa kigeni ni lazima wawe wanachezea timu ya Taifa au klabu za
Ligi Kuu huko wanakotoka.
Kanuni hiyo inasema: “Klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni
wa ngazi ya kimataifa ambao ni wa timu za Taifa na Ligi Kuu kutoka nje ya nchi
wasiozidi watano (5).
Wachezaji kutoka Ulaya na Marekani ya Kusini wanweza kuwa wa daraja
la pili na kuendelea, na klabu inaruhusiwa kuchezesha wachezaji walioorodheshwa
wasiozidi watano (5) wa kigeni katika mchezo mmoja. Wachezaji hao watasajiliwa
baada ya TFF kuhakikisha usahihi wa taarifa zao na kukamilika kwa taratibu za
uhamisho wa kimataifa.”
No comments:
Post a Comment