Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linampongeza Amani Ibrahim Makungu kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa
Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) katika uchaguzi uliofanyika juzi (Juni
30 mwaka huu) kwenye hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar.
Ushindi wa asilimia 94
alioupata Makungu ambaye hakuwa na mpinzani katika uchaguzi huo mdogo unaonesha
imani ambayo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA wanayo kwake katika kukiongoza chama
hicho.
Ni matarajio ya TFF kuwa
ushindi huo utatafsiriwa kwa vitendo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA na wadau
wa mpira wa miguu Zanzibar kwa kumpa Makungu ushirikiano wa asilimia 100 ili
kuhakikisha Kamati yake ya utendaji inafanya kile kinachotarajiwa na
wengi.
Makungu si mgeni katika mpira
wa miguu, na mchango aliotoa kwa mchezo huo visiwani kabla ya kuwania nafasi
hiyo unatambuliwa na kila anayefuatilia maendeleo ya mpira wa miguu katika
Zanzibar.
TFF tunaahidi kuendelea kutoa
ushirikiano kwa ZFA chini ya Makungu kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Ali
Ferej Tamim ili kuhakikisha ustawi wa mpira wa miguu visiwani Zanzibar na
Tanzania kwa ujumla.
MISRI YAAHIRISHA MECHI DHIDI
YA NGORONGORO HEROES
Mechi mbili za kirafiki kati
ya timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro
Heroes) na Misri zilizokuwa zichezwe mwezi huu zimefutwa.
Chama cha Mpira wa Miguu Misri (EFA) kimetuma
taarifa jana (Julai 1 mwaka huu) kikiomba kusogezwa mbele hadi mwishoni mwa
Agosti baada ya kushindwa kupata usafiri wa ndege kuwahi tarehe ambazo
ilikubaliana na TFF kwa ajili ya mechi hizo.
Ngorongoro Heroes ambayo
tayari iko kambini ilikuwa icheze mechi hizo Julai 3 na 5 mwaka huu jijini Dar
es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi kabla ya kuikabili Nigeria katika mechi
ya michuano ya Afrika, Julai 29 mwaka huu.
Mechi nyingine za kirafiki
kwa Ngorongoro Heroes inayofundishwa na Jakob Michelsen zitachezwa Julai 14 na
16 mwaka huu dhidi ya Rwanda.
RUVUMA YAIFANYIA MAUAJI LINDI
7-2
Timu ya Ruvuma imethibitisha
kuwa mwiba mkali katika michuano ya Copa Coca-Cola mwaka huu baada ya leo
asubuhi (Julai 2 mwaka huu) kuishushia Lindi kipigo cha mabao 7-2.
Hadi mapumziko kwenye mechi
hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani, washindi ambao kwa
matokeo hayo wamejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza 16 bora walikuwa mbele
kwa mabao 3-0.
Waliotikisa nyavu ni Anthony
Christian dakika ya 23 na 50, Edward Songo dakika ya 27, 75 na 86 na Sunday
Leonard dakika ya 32 na 60. Mabao ya Lindi yalifungwa na Salum Mnyamwile dakika
ya 18 kwa njia ya penalti na lingine dakika ya 48 kupitia kwa Mwarami Maundu.
Nayo Tanga imepata ushindi
wake wa kwanza katika michuano hiyo baada ya kuifunga Manyara mabao 2-0 katika
mechi ya kundi B iliyochezwa Uwanja wa Tamco mkoani Pwani. Mabao ya washindi
yalifungwa na Mbwana Musa dakika ya 47 na Issa Mwanga dakika ya 60.
Katika mechi tatu
zilizotangulia Tanga ilitoka sare ya mabao 3-3 na Morogoro, ikapata sare
nyingine ya 1-1 dhidi ya Mwanza, na baadaye 1-1 na Tanga.
Kagera imeendelea kujitutumua
katika michuano hiyo baada ya kupata ushindi wake wa pili katika kundi D kwa
kuilaza Kusini Unguja bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tanganyika
Packers ulioko Kawe jijini Dar es Salaam.
Bao lake lilifungwa dakika ya
76 na Novati Sebastian. Mechi iliyopita Kagera iliifunga Tabora mabao 2-0 baada
ya kuteleza katika mechi mbili za kwanza kwa kufungwa na Kilimanjaro na
Singida.
Mechi nyingine ilichezwa
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam ambapo Kinondoni iliibuka na
ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mara.
UONGOZI TWIGA STARS WATOA
TAMKO
Uongozi wa Twiga Stars
umekana kuwepo vitendo vyovyote vya kinyume na maadili kwa wachezaji wa timu
hiyo ambayo hivi karibuni ilitolewa kwenye mechi za mchujo za michuano ya Afrika
kwa Wanawake (AWC).
Wakizungumza na waandishi wa
habari leo (Julai 2 mwaka huu), Meneja wa Twiga Stars, Furaha Francis na
aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa wamesema hakuna
vitendo vya aina hiyo.
Mkwasa amesema alikaririwa
vibaya kuhusu suala hilo wakati akiwa kwenye mahojiano na kituo cha televisheni
cha Star Tv kutokana na swali alilokuwa ameulizwa kuhusiana na vitendo
hivyo.
“Ukifuatilia mahojiano yangu
na Star Tv mimi sikusema kuwa kuna vitendo hivyo. Tatizo nadhani lilianzia kwa
magazeti yaliyonukuu kupitia Star Tv, na wala kujiuzulu kwangu hakukuhusiana na
hilo, nimewajibika kama kocha kutokana na kutolewa na Ethiopia,” amesema
Mkwasa.
Naye Furaha Francis amesisitiza kuwa hakuna
vitu vya aina hiyo katika timu hiyo, na kama kuna mtu ana ushahidi na hilo ni
bora akauonesha badala ya kuzungumzia uvumi kuliko ukweli.
“Ukweli ni kwamba si sisi na
wachezaji tu ambao hatukufurahishwa kutolewa na Ethiopia, wapo Watanzania wengi
ambao hawakufurahishwa na matokeo yale. Twiga Stars si timu ya kudumu, haikai na
wachezaji kwa muda wote, kila mchezaji ana timu yake.
“Madai yanayoenezwa na baadhi
ya vyombo vya habari kuhusu vitendo hivyo yametuchafua sana. Tunaomba kama kuna
mtu ana ushahidi na hilo atueleze kuliko kuendelea kutuchafua,” amesema.
No comments:
Post a Comment