Wednesday, June 13, 2012

TAIFA STARS YAJIPANGA KUIKABILI MSUMBIJI

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema ili kuitoa Msumbiji ‘Mambas’ kwenye michuano ya Afrika ni lazima timu yake ishinde mechi ya marudiano itakayochezwa Juni 17 mwaka huu jijini Maputo.

Mechi ya marudiano kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa ulioko Zampeto nje kidogo ya Jiji la Maputo kuanzia saa 9 mchana kwa saa za huko.

Kim amewaambia Waandishi wa Habari leo (Juni 13 mwaka huu) kuwa maandalizi ya kikosi chake yanakwenda vizuri ingawa ana wachezaji watatu ambao ni majeruhi; kipa Mwadini Ali, na mabeki Nassoro Masoud Cholo na Waziri Salum.

Amesema wachezaji hao hawatakuwemo kwenye msafara wa timu hiyo utakaoondoka Juni 15 mwaka huu saa 11 alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.

Kocha huyo amesema baada ya mechi tatu maendeleo kiuchezaji kwa timu yake inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ni mazuri ingawa bado anafanyia kazi kwa nguvu safu ya ushambuliaji. Mechi iliyopita Taifa Stars iliifunga Gambia 2-1 huku mabao yote yakifungwa na mabeki.

Iwapo Taifa Stars itaitoa Msumbiji katika raundi ya mwisho itapangiwa moja kati ya timu 16 zilizocheza Fainali za AFCON zilizofanyika Januari mwaka huu katika nchi za Gabon na Equatorial Guinea. Katika mechi ya kwanza dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Dar es Salaam, Februari 29 mwaka huu timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Taifa Stars ambayo msafara wake utakuwa na wachezaji 20 itaagwa kesho (Juni 14 mwaka huu) saa 6 mchana kambini kwao- hoteli ya Accommondia (Tansoma) jijini Dar es Salaam.  Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa ajili ya kujenga afya kupitia mpira wa miguu.

KUONA TWIGA STARS, ETHIOPIA 2,000/-
Kiingilio cha chini kwa mechi ya kufuzu kwa fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Ethiopia itakayochezwa Jumamosi (Juni 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 2,000.

Kiwango hicho ni kwa washabiki kwa viti vya bluu, kijani na rangi ya chungwa. Viti hivyo kwa pamoja vinachukua jumla ya watazamaji 48,590 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua washabiki 60,000.

Viingilio vingine kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni ni sh. 5,000 kwa VIP B na C wakati VIP A itakuwa sh. 10,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi kuanzia saa 3 asubuhi.

Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi Grace Msiska atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake ni Bernadettar Kwimbira, Happiness Mbandambanda na Linda Chikuni, wote kutoka Malawi. Kamishna ambaye anatoka Kenya ni Maqulate Atieno. Waamuzi hao wanawasili leo.

WAAMUZI KOZI YA FIFA KUPIMWA UFAHAMU WA ALAMA
Waamuzi 54 wanaoshiriki kozi ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) iliyoanza Juni 11 mwaka huu, kesho (Juni 14 mwaka huu) watahamia Uwanja wa Karume kwa ajili ya mazoezi ya alama (signals). Mazoezi hayo yatafanyika kuanzia saa 1-4 asubuhi.

Kozi hiyo itakayomalizika kesho (Juni 14 mwaka huu) inaendeshwa na wakufunzi Carlos Henriques na Mark Mizengo kutoka FIFA wakisaidiwa na wakufunzi wengine wanne wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Wakufunzi wa TFF ni Kapteni mstaafu Stanley Lugenge, Leslie Liunda, Soud Abdi na Riziki Majala.

Waamuzi wanaoshiriki ni 14 wa Tanzania wenye beji za FIFA ambao ni Erasmo Jesse, Ferdinand Chacha, Hamis Changwalu, Hamis Maswa, Israel Mujuni, John Kanyenye, Josephat Bulali, Judith Gamba, Mwanahija Makame, Oden Mbaga, Ramadhan Ibada, Saada Tibabimale, Samuel Mpenzu na Sheha Waziri.

Washiriki wengine ni 20 wa daraja la kwanza (class one), kati ya hao watano wanatoka Zanzibar. Lakini vilevile wapo waamuzi chipukizi (watoto) 20 ambao mwaka jana walitumika katika michuano ya Kombe la Uhai na Copa Coca-Cola.

No comments:

Post a Comment