Tuesday, September 11, 2012

TWITE, YONDAN WAIDHINISHWA YANGA

KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inayoongozwa na Mwenyekiti , Alex Mgongolwa, jana usiku imewaidhinisha wachezaji Mbuyu Twite na Kevin Yondan kuchezea Yanga katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, unaoanza mwishoni mwa wiki hii.

 Kamati hiyo, iliyokaa zaidi ya mara mbili kwa kuzikutanisha Simba na Yanga, zilizokuwa na madai ya kila mmoja kutaka wachezaji hao waiidhinishwe katika timu zao, ilifikia maamuzi hayo jana kwa Yanga kupewa siku 21 kulipa dola 32,000 ambazo Simba SC ilimlipa Twite ili ajiunge nao, lakini baadaye akaghairi na kusaini na kuhamia Yanga.

 Habari za ndani katika kikao hicho, wajumbe walihoji iweje Simba wamteke Kelvin Yondan juzi usiku na kumlazimisha kusaini Simba huku wakiwa na madai kuwa mchezaji huyo alikwisha saini Simba?.

 Katika tukio hilo linalomhusisha mchezaji wa zamani wa Simba na kiongozi wa ngazi za juu wa timu hiyo, halifanikiwa na Yondan alitoa taarifa Polisi za kutekwa na kupewa RB ya kumsaka aliyempeleka Simba bali matakwa yake.

 Katika kikao, cha pamoja baina ya Simba na Yanga Jumatatu kilichovunjika bila kufikia makubaliano kuhusu mustakabali wa wachezaji hao kutokana na kila mmoja kudai ni halali upande wake.

 Katika kikao hicho kilichoanza majira ya saa 7:00 mchana, hoja ya kwanza kuwasilishwa mezani ilikuwa ni suala la beki Twite na upande wa Yanga uliwakilishwa na Sanga na Katibu, Celestine Mwesigwa wakati kwa Simba walikuwepo Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe.

 Ikumbukwe, Simba iliwasilisha malalamiko ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa Twite. Ilidai Twite alisaini mkataba na klabu yao Agosti 1, mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine 2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo, mchezaji huyo akahamia Yanga.

 Katika mjadala huo, Simba ilikubali kurudishiwa fedha zao, lakini viongozi wa Yanga wakasema hawawezi kutoa hadi waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alisema viongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.

 Simba wakasema kauli yake ya Rage ilikuwa sehemu ya utani wa jadi, kama ambavyo Yanga walimvalisha jezi Twite yenye jina la Rage. Kufikia hapo, Simba wakasema hawawezi hata kujadili suala la Kevin Yondan na Kamati ya Mgongolwa ikasema itapitia maelezo ya pande zote, watatoa majibu kwa mujibu wa kanuni na sheria Septemba 10, mwaka huu, yaani leo.

 Katika kesi ya Yondan, walalamikaji ni Simba, ambao wanadai beki huyo alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba na klabu yao.Awali, Kamati ya Mgongolwa ilikutana Jumapili iliyopita asubuhi hadi usiku, bila kupata suluhisho la pingamizi hizo na kuamua kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata suluhu siku iliyofuata.

 

No comments:

Post a Comment