Monday, August 20, 2012

Tanzania chali Miss World

MWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya urembo ya Dunia 2012, Lisa Jensen jana aliungana na warembo wengine 18 waliomtangulia kutoka Tanzania, kupigwa kumbo katika fainali hizo, baada ya mrembo wa China, Yu Wenxia  kutwaa taji hilo katika shindano lililofanyika Ordos Stadium Arena kaskazini mashariki ya jiji la kibiashara la Ordos.
Zilikuwa kelele zilizopitiliza baada ya mashabiki kushuhudia mrembo kutoka katika ardhi yao akitwaa taji hilo la 62, lililokuwa likishikiliwa na mrembo wa  Venezuela, Ivian Sarcosa ambaye jana alimvika taji malkia huyo mpya wa dunia katika mashindano yaliyoshirikisha nchi 116 kwa mara ya kwanza.
"Nikiwa mdogo nilisaidiwa na watu wengi sana, jambo ambalo ni fursa kwangu nami kufanya hivyo baada ya kutwaa taji hilo, ni bahati kubwa maishani mwangu", alisema Yu mbele ya waandishi wa habari akihojiwa kuhusu ushindi wake.
Sudan Kusini iliyoshiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza imefanya maajabu kwa kuingia hatua ya fainali ya mwisho kabisa ya saba bora. Katika 15 Kenya nayo ilitinga hatua hiyo ikiwa na  Sudani Kusini. Nchi za India,Mexico, Australia, Jamaica,China ,Wales, Uingereza, Brazil,Uhispania,Phillipines, Marekani, Uholanzi na Indonesia, nazo zilifika hatua hiyo.
Mbali ya China, ushindi wa pili ulikwenda kwa mrembo wales, Sophie Moulds wakati nafasi ya tatu ilikwenda kwa mrembo wa Australia, Jessica Kahawaty.  Taji hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1951 lilitwaliwa na  Kiki Hakansson wa Sweden.Venezuela imewahi kutoa mrembo wa dunia mara sita wakati India na Uingereza zinafuatiwa kwa kutwaa mara tano.
Warembo wengine waliopata kushiriki miss World na miaka yao kwenye mabano ni pamoja na Aina Maeda(1994), Emilly Adolf(1995), Shose Sinare(1996), Saida Kessy(1997), Basila Mwanukuzi(1998), Hoyce Temu(1999), Jacquline Ntuyabaliwe 'K-Lyne'(2000),  Happiness Sosthnes Magese (2001), Angela Damas Mutalimwa(2002) na Sylvia Remmy Bahame(2003).
Wengine ni Faraja Kotta(2004), Nancy Sumari(2005), Wema Sepetu(2006), Richa Adhia(2007), Nasreem Karim(2008), Miriam Gerald(2009), Genevieve Emmanuel Mpangala(2010) na Salha Israel anayelishikilia taji hilo ambalo anatarajiwa kuanza kulivua Oktoba.
mwisho

No comments:

Post a Comment