Thursday, August 16, 2012

FINALI MISS WORLD 2012 KESHO

TANZANIA kesho inatupa karata yake nyingine katika mashindano ya kimataifa, kwa mwakilishi wake, Lisa Jensen kupanda jukwaani Ordos Stadium Arena kuwania taji la urembo wa dunia, akichuana na vimwana kutoka nchi 116.                                                                        Mashindano hayo ya 61 tangu kuanzishwa kwake, yatavunja rekodi ya idadi kubwa ya washiriki tangu yaanzishwe kwake ambapo Lisa Jensen anaiwakilishi nchi kwa mara ya 19 tangu kufanyika na kupeleka mwakilishi wake mwaka 1994.Miss World iliyoanzishwa mwaka 1951 kwa kushirikisha warembo 26 jukwaani jijini London Uingereza, chini ya uratibu wa marehemu Eric Morley kesho warembo 116 wanapanda jukwaani Ordos Stadium Arena, China ikiwa chini ya uratibu wa mke wa mwanzilishi huyo, Julia Morley.Kwa mujibu wa mtandao wa waandaji hao, nchi zipatazo 160 duniani, zinatarajiwa kutazama moja kwa moja mashindano hayo kupitia luninga, hiyo  ikimaanisha mamilioni ya watu duniani wanatarajia kuona mashindano hayo.
Lisa ambaye aliingia kati ya warembo 45 katika kategoria ya mitindo, mbali ya kuwa mrembo wa 19 kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo, lakini ana deni kubwa la mafanikio pekee ya Miss Tanzania 2005, Nancy Sumary aliyeingia sita bora ya mashindano hayo na kutwaa taji la Miss World Afrika.
Rekodi hiyo haijafikiwa na mrembo yeyote tangu Tanzania ianze kupeleka mwakilishi wakemwaka 1994 kupitia Aina Maeda. Lisa ambaye alipata nafasi hiyo katika shindano dogo la second chance lililoshirikisha warembo waliopata kushiriki Miss Tanzania katika miaka tofauti kuanzia 2006 alioshiriki yeye, mwaka ambao Wema Sepetu alishinda, nafasi ya pili kutwaliwa na Jokate Mwegelo na Lisa wa tatu.
Kufanyika shindano hilo dogo, kumebadilisha ratiba ya Miss Tanzania mwaka huu, ikimaanisha mshindi wa mwaka huu katika shindano litakalofanyika katikati ya mwezi Oktoba, ataandaliwa kwa mwaka mzima kwa ajili ya shindano la dunia mwakani 2013.
Hiyo itakuwa ni nafasi kubwa kwa Tanzania kupata muda mrefu wa maandalizi, jambo ambalo limekuwa likifanyika katika nchi nyingi ambazo zimepata kufanikiwa katika mashindano hayo. Hii pia ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupeleka Miss Tanzania ambaye hakuvikwa taji na mrembo anayemaliza muda wake kutoka na mataji hayo kutofautiana.
Warembo wengine waliopata kushiriki miss World na miaka yao kwenye mabano ni pamoja na Aina Maeda(1994), Emilly Adolf(1995), Shose Sinare(1996), Saida Kessy(1997), Basila Mwanukuzi(1998), Hoyce Temu(1999), Jacquline Ntuyabaliwe 'K-Lyne'(2000),  Happiness Sosthnes Magese (2001), Angela Damas Mutalimwa(2002) na Sylvia Remmy Bahame(2003).
Wengine ni Faraja Kotta(2004), Nancy Sumari(2005), Wema Sepetu(2006), Richa Adhia(2007), Nasreem Karim(2008), Miriam Gerald(2009), Genevieve Emmanuel Mpangala(2010) na Salha Israel anayelishikilia taji hilo ambalo anatarajiwa kuanza kulivua Oktoba.
mwisho

No comments:

Post a Comment