Sunday, July 22, 2012

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA DOREFA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Julai 21 mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa DOREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Dodoma.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya DOREFA chini ya uenyekiti wa Nasoro Kipenzi ambaye amechaguliwa kwa kipindi cha pili mfululizo.
 
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Dodoma kwa kuzingatia katiba ya DOREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya DOREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo uliofanyika hoteli ya Dear Mama ni Nassoro Kipenzi (Mwenyekiti), Thadeo Kaliza (Makamu Mwenyekiti), Stewart Masima (Katibu Mkuu), Kepha Maswaga (Mhazini), Mulamu Ngh’ambi (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Mohamed Aden (Mwakilishi wa Klabu TFF), Zawdi Kassim (Mjumbe Kamati ya Utendaji).

 
RAMBIRAMBI MSIBA WA MTANGAZAJI JOSEPH MAPUNDA
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mtangazaji wa michezo wa Radio Wapo, Joseph Mapunda kilichotokea juzi asubuhi (Julai 21 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Mapunda alifanya kazi na TFF kwa kuripoti shughuli zetu nyingi za mpira wa miguu, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mapunda, Radio Wapo na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TASWA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Mapunda mahali pema peponi. Amina

No comments:

Post a Comment