Thursday, September 6, 2012

COPA TANZANIA YAWA YA PILI AFRIKA KUSINI


Kombaini ya Tanzania ya Copa Coca-Cola imeshika nafasi ya pili katika kambi ya kimataifa ya michuano hiyo inayoendelea jijini Pretoria, Afrika Kusini. Tanzania imemaliza mechi za kambi hiyo kwa kufikisha pointi 14.

Ilicheza mechi yake ya mwisho jana (Septemba 5 mwaka huu) dhidi ya Malawi na kutoka suluhu, matokeo yaliyoifanya ifikishe pointi 14.

 Zambia ndiyo iliyokamata nafasi ya kwanza kwa kufikisha pointi 15.

Mechi hizo zilichezwa kwa mtindo wa ligi baada ya nchi nyingine kushindwa kwenda Afrika Kusini kutokana na kuchelewa kupata viza za kuingia za kuwawezesha kuingia nchini humo.

 Mbali ya Tanzania, nchi nyingine zilizowahi kambi hiyo ni Kenya, Uganda, Nigeria, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe, Zambia na timu mchanganyiko katika kambi hiyo (CEWA). Katika mechi zake Tanzania ilitoka suluhu na Nigeria, ikafungwa 3-2 na Kenya, ikaichapa Zimbabwe 3-0, ikailaza CEWA 3-0, ikaifunga Msumbiji 2-0, ikashinda 2-0 dhidi ya Uganda na ikafungwa 1-0 na Zambia.

 Wachezaji wawili wa Tanzania wamechaguliwa kwenye kombaini ya kambi hiyo (Dream Team). Wachezaji hao ni mfungaji bora Basil Seif ambaye ana mabao sita na kipa bora Tumaini Baraka. Pia Sylvester Marsh wa Tanzania amechaguliwa kuwa kocha bora katika kambi hiyo.

Makocha watano kutoka timu ya Chelsea ya Uingereza wanaanza kutoka mafunzo leo (Septemba 6 mwaka huu) ambapo yatamalizika kesho (Septemba 7 mwaka huu) na timu zitarejea nyumbani Septemba 8 mwaka huu. k.

Robert Luke Udberg, Russel William Banyard, Oliver Staurt Woodall, Shane Jason Hughes na Dean Aaron Steninger kutoka Chelsea FC Foundation ndiyo wanaounda jopo hilo la makocha.

 
MKATABA WA UDHAMINI KUSAINIWA SEPT 11

Mkataba wa udhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo itadhaminiwa tena Vodacom utasainiwa Jumanne (Septemba 11 mwaka huu) kwenye ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.

Taarifa rasmi juu ya muda wa kusaini na pande zitakazoshuhudia hafla hiyo itatolewa hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment