Monday, July 16, 2012

CRDB YASHINDA TENDA YA TIKETI ZA ELEKTRONIKI

Benki ya CRDB PLC imeibuka mshindi wa tenda ya kutengeneza tiketi za elektroniki za kuingilia uwanjani iliyotangazwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kampuni saba zilijitokeza katika hatua ya awali ya kuonesha nia (Expression of Interest) kwa ajili ya tenda hiyo ambapo Aprili 19 mwaka huu Kamati ya Mipango na Fedha ya TFF ambayo ndiyo Bodi ya Tenda ya shirikisho ilipitia maombi hayo na kupitisha nne kati ya hizo.

Baadaye kampuni hizo nne; CRDB Bank PLC, Prime Time Promotions, Punchlines (T) Limited na SKIDATA People Access Inc. zilitakiwa kuwasilisha rasmi tenda zao zikionesha jinsi zitakavyofanya shughuli hiyo pamoja na gharama ya utengenezaji kwa tiketi moja.

Bodi ya Tenda ya TFF ilikutana Julai 13 mwaka huu kwa ajili ya kupitia tenda hizo ambapo kampuni zote nne zilifanya uwasilishaji (presentation) wa jinsi zitakavyofanya shughuli hiyo, na baadaye kuipa kazi hiyo benki ya CRDB.

Uamuzi huo wa Bodi ya Tenda uliwasilishwa mbele ya Kamati ya Utendaji ya TFF. Kamati ya Utendaji ya TFF katika kikao chake kilichofanyika Julai 14 mwaka huu iliridhia uteuzi huo wa benki ya CRDB.

Baadhi ya vigezo ambavyo Bodi ya Tenda ya TFF iliangalia na kuipa CRDB tenda ni uwezo wa kufanya kazi hiyo (capacity), hadhi yake mbele ya jamii (credibility) katika shughuli inazofanya na teknolojia ya kisasa itakayotumika kutengeneza tiketi hizo.

Uamuzi wa TFF kutangaza tenda hizo ulilenga kuimarisha udhibiti wa mapato ya milangoni na kurahisisha mtiririko mzima wa washabiki kupata tiketi na kuingia viwanjani.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema: “Hatua hii ni muhimu sana, kwani tulikuwa tukiisubiri kwa muda mrefu. Si tu itaimarisha udhibiti wa mapato, bali pia itaondoa matatizo ya tiketi na kuendelea kujenga credibility (kuaminika) ya TFF. Mafanikio haya si kwa TFF pekee bali mpira wa miguu kwa ujumla.”

CRDB imeanza mara moja mchakato wa shughuli hiyo ambapo tiketi hizo zinatarajia kuanza kutumika rasmi katika kipindi cha kati ya miezi miwili na mitatu kuanzia sasa.

No comments:

Post a Comment